Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga yupo nchini Italia kuhudhuria Mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Afrika na  Italia  (Italy – Africa Ministerial Conference) uliofanyika  tarehe 18 Mei 2016 katika ukumbi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ambapo masuala mengi ya ushirikiano kati ya Afrika na Italia yalizungumzwa. Kati ya masuala hayo ni pamoja na fursa mbalimbali za uwekezaji katika sekta ya kilimo na nishati na namna zinavyoweza kuinua uchumi wa nchi za Afrika.


italia barabara iringa1
Mhe. Dkt. Augustine P.Mahiga (MB), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akichangia mada kwenye mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Afrika na Italia

Mhe. Mahiga alipata fursa ya kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Italia, Mhe. Paolo Gentiloni ambapo walizungumzia masuala ya ushirikiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Italia. Mhe. Waziri Mahiga pamoja na mambo mengine aliomba Serikali ya Italia kuendelea kufadhili miradi iliyokuwa inatekelezwa na Serikali hiyo katika siku za nyuma ikiwemo  sekta ya kilimo, afya na miundombinu. Aidha, Mhe. Waziri Mahiga aliwasilisha miradi ya ujenzi wa barabara ili kuona uwezekano wa Serikali ya Italia kuifadhili miradi hiyo. Pia Waziri Mahiga alimuomba Waziri Gentiloni kuangalia uwezekano wa kukarabati hospitali ya Ipamba iliyoko Iringa ambayo imechakaa sana. Hospitali hiyo ilianzishwa na Wamisionari wa Shirika la Wakonsolata wa Italia.
Kwa uapande wake Waziri Gentiloni alipokea maombi hayo na kuahidi kuyafanyia kazi.


italia barabara iringa2
Mhe. Dkt. Augustine P.Mahiga (MB), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akiwa kwenye picha ya pamoja na Mhe. Mhe Paolo Gentiloni, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Italia kabla ya mazungumzo ya pande mbili.